Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali yafuatayoNatunga nikiwaasa, msije kujijutia, Mitego sije wanasa, mkaja kuangamia, Tamaa nyingi za pesa, gereza zitawatia, Kila mpenda rushuwa, jela inamkonyeza. Jela inakukonyeza, kama hutajizuwia, Haina ndugu gereza, jela si kuchezea, Inajuvya na kupoza, wenye nguvu kutulia, Kila mpenda rushuwa, jela inamkonyeza. Rushuwa si kitu chema, walaji jihadharini, Mkila zitawakwama, zitawatoka puwani, Wazilao hulalama, si mimi ila Fulani, Kila mpenda rushuwa, jela inamkonyeza. Ridhika na upatacho, kama moja au mbili, Usitaraji mkocho, apatao Bwana Ali, Tamaa zako za macho, zitakuletea mbuli, Kila mpenda rushuwa, jela inamkonyeza. Nimeona kemu kemu, wenye vyeo kutimia, Maleba wakiwahimu, rushuwa kuwaletea, Muogopeni Karimu, beba haombwi rushuwa, Kila mpenda rushuwa, jela inamkonyeza. Kuna wengi mahakimu, haki wanazopinduwa, Yatima kuwadhulumu, kwa kupapia rushuwa, Kwa kutaka darahimu, aso haki anapewa, Kila mpenda rushuwa, jela inamkonyeza. MASWALI (a) Andika anwani mwafaka kwa utungo huu. (alama 2) (b) Taja athari tatu za rushwa kama zilivyoelezwa katika shairi. (alama 3) (c) Ni nini msimamo wa mwandishi kuhusu rushwa? (alama 2) (d) Andika ubeti wa pili katika lugha sufufu. (alama 4) (e) Eleza sifa nne zinazotambulisha utungo huu kuwa ni shairi. (alama 4) (f) Huku ukitoa mifano, onyesha namna uhuru wa mshairi unatanda katika shairi hili. (alama 2) (g) Eleza msamiati ufuatao kama ulivyotumika katika shairi. (alama 3) (i) Kupapia (ii) Nikiwaasa (iii) Inamkonyeza MAJIBU
(a) Ufisadi/Rushwa 1 x 2 = 2 (b) Athari za rushwa Kutiwa gerezani Kutofaidi chochote Kulalamika 3 x 1 = 3 (c) Msimamo wa mwandishi kuhusu rushwa ni kuwa ni jambo lisilofaa tujiepushe nalo 1 x 2 = 2 (d) Ubeti wa 2 – Lugha ya nathari. Usipojizuia na ukaendelea kula rushwa utafungwa. Huko gerezani hakuna ndugu wala mzaha. Tena wenye nguvu hawatambuliwi na nguvu zao ni bure. Yeyote anayekula rushwa hatimaye atajikuta gerezani. 4 x 1 = 4 (e) Sifa nne kuonyesha ni ushairi Limepangika katika beti Lina mishororo minne kwenye ubeti Lina vipande viwili kwenye mshororo Kila mshororo una vina viwili mwishoni mwa vipande (ukwapi na utao) Mshororo wa mwisho umekaririwa (kibwagizo) Lugha iliyotumika ni ya mkato Utoshelezi upo zozote 4 x 1 = 4 (f) Uhuru wa mshairi Inkisari (ufupishaji wa maneno) Mfano sije – msije Aso – asiye Mazida (kurefusha) K.m rushuwa – rushwa Muogopeni – mwogopeni Tabdila k.m. puwani – puani Kuboronga sarufi mfano. Nyingi pesa – pesa nyingi Gereza ziwatia – zitawatia gerezani zozote 2 x 1 = 2 Utohozi – maleba (g) (i) Kupapia – kuendea kitu kwa hamu kubwa (ii) Nikiwaasa – nikiwaonya, nikiwakataza (iii) Inamkonyeza – inamwita/ inatoa ishara ya kuita / inamvuta. 3 x 1 = 3
0 Comments
Leave a Reply. |
AuthorAtika School Team Archives
December 2023
Categories
All
|
Can't find what you are looking for? Don't worry, Use the Search Box Below.
Primary Resources
College Resources
|
Secondary Resources
|
Contact Us
Manyam Franchise
P.O Box 1189 - 40200 Kisii Tel: 0728 450 424 Tel: 0738 619 279 E-mail - sales@manyamfranchise.com |